Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka Maafisa Habari nchini kutambua kuwa utoaji wa habari kwa wananchi kwa sasa siyo utashi tena bali ni sheria.
Waziri Mwakyembe ameyasema hayo leo, Jumatatu, jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha maafisa habari kwa mwaka 2018, ambacho kimebeba kauli mbiu isemayo, ” Je, Mawasiliano ya Kimkakati Yanachagiza vipi Tanzania ya Viwanda?
Waziri Mwakyembe amesema kwa sasa Tanzania inahitaji Afisa Habari anayejituma, anayehuisha tovuti yake na kuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya habari vinavyomzunguka.
“Serikali inatarajia kuwa maafisa mawasiliano serikalini mtakuwa wabunifu na kuwapatia wananchi haki yao ya msingi ya kupata taarifa”. alisema Waziri Dkt. Mwakyembe.
Naye Msemaji mkuu wa Serikali, Hassan Abbas amesema, anaamini mara baada ya kikao kazi hicho, maafisa mawasiliano hao wataweza kuenenda kimkakati na kufanya kazi kwa bidii na kisasa kwa manufaa ya taasisi zao.
Akizungumza kwenye kikao kazi hicho, Mratibu mkazi wa Umojawa Mataifa (UN), Alvaro Rodriguez amesema, UN inaiona Tanzania ya leo na kesho yenye mafanikio makubwa kupitia kilimo,vita dhidi ya rushwa, elimu bure na kasi ya ukuaji wa uchumi wa kati kupitia viwanda.