Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezitaka taasisi zinazosimamia biashara kuhakikisha zinaondoa urasimu na kuwawezesha wafanyabiashara nchini kwa kuwekea mazingira rafiki ya biashara zao.
Dkt. mwinyi ameyasema hayo wakati akifunga Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam katika ukumbi wa Rashid Mfaume Kawawa, uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitashirikiana katika kuhamasisha ukuaji wa biashara na uwekezaji kwa kufanyia kazi maoni ya wafanyabiashara nchini.
Aidha, Dkt. Mwinyi pia ameongeza kuwa wataboresha mazingira ya biashara kwa kuwezesha taasisi za Serikali kuwa na mifumo inayosomana itakayoweza kupunguza gharama zisizo za lazima na kuondoa utitiri wa tozo katika biashara nchini.
Maonesho hayo ya 47 kwa mwaka huu yameshirikisha jumla la kampuni 3500, kampuni 267 ni kampuni za nje ya Nchi kutoka Nchi 17 na kutembelewa na wananchi takribani Milioni 3.