Waziri wa Mambo ya Ndani, Dkt. Mwigulu Nchemba ameteketeza jumla ya ekari sita za bangi zilizokuwa zimelimwa katikati ya msitu ndani ya kijiji cha Engalaoni wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Akishirikiana na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha, (RPC) Charles Mkumbo pamoja na vikosi vya askari wa jeshi la polisi mkoani humo walilazimika kuacha magari yao njiani na kutembea umbali wa kilomita 5 milimani ili kufika katikati ya msitu huo ambapo wamiliki wa mashamba hayo walitokomea kusikojulikana.
Aidha, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi hilo Mwigulu amesema kuwa serikali itaendelea na oparesheni pande zote za nchi na haitasita kuwakamata wahusika wote na kutaifisha magari yatakayotumika kusafirisha bangi.
Hata hivyo, Dkt. Nchemba amewapongeza askari walihusika katika Operesheni hiyo na kuwataka waongeze juhudi za kupambana na wakulima bangi katika maeneo yote yanayolimwa bangi nchini.