Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein ameridhishwa na ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 3.6 kutoka eneo la kwa Mabata hadi Kijitoupele, mkoa wa Mjini Magharibi inayoondoa kero ya usafiri katika eneo hilo.
Rais Shein amekagua ujenzi wa barabara hiyo leo Agosti 21, 2017 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu mkoani humo, ambapo amewashukuru wananchi kwa kukubali nyumba zao kuvunjwa kupisha ujenzi wa barabara hiyo ili kuondoa kero ya usafiri kwa maslahi ya wote.
Amesema awali hakuamini maelezo aliyopewa na Mkuu wa Mkoa huo, Ayoub Mohamed Mahmud kuwa wananchi wangepisha mradi huo, lakini sasa ameona utekelezaji wake kwa vitendo.
Aidha, Dkt. Shein ameagiza idara za Ofisi yake kuhakikisha zinatoa kwa wakati kiasi cha shilingi milioni 900 zilizosalia ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Amewataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi akieleza kuwa haiwezi kuahidi isitekeleze, huku akiwanyooshea kidole waliobeza ahadi hiyo ya Serikali kwa wananchi.
“Wapo waliokejeli na kutubeza kuwa hatutaweza, kwamba ‘aah wapi hawa watapata wapi fedha, wataweza wapi hawa’; na wapo walioamini kuwa Serikali itajenga kwa ubora na umakini mkubwa, “amesema Dkt. Shein.
“Serikali hii inayoongozwa na CCM haiwezi kuahidi kitu isitekeleze,” ameongeza.
Dkt. Shein amewataka wanaotumia vyombo vya usafiri kufuata sheria za barabarani kwani barabara hiyo inapita karibu na makazi ya watu.
Amesema bila kufuata sheria na madereva kuwa makini, maisha ya watoto, wazee na walemavu yatakuwa hatarini katika barabara hiyo.
Hivyo, Rais Shein amewataka wananchi kushirikiana na jeshi la polisi kuwa walinzi dhidi ya madereva wasiozingatia sheria za barabarani. Hata hivyo, aliwataka kuhakikisha wanafanya ulinzi huo bila kuchukua sheria mikononi.
Rais Shein anakamilisha leo ziara yake ya kikazi mkoa wa Mjini Magharibi, ziara aliyoianza Jumamosi, Agosti 19.