Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, amewahakikishia wanadiaspora kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasimamia na kuhakikisha kuwa sheria ya Diaspora inakamilika kabla ya mwezi Mei, 2020.
Rais Dkt. Shein ametoa kauli hiyo leo mjini Zanzibar wakati alipokuwa akifungua rasmi kongamano la sita la Diaspora ambalo limeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi-Zanzibar.
“Kutokana na kutambua umuhimu wa watanzania waishio nje ya nchi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliunda idara maalumu ya kushughulikia masuala ya Diaspora katika wizara ya Mambo ya nje mwaka 2010 ili kutekeleza kwa vitendo azma yetu ya kuwashirikisha wanadiaspora Tanzania katika kuendeleza nchi yetu” amesema Dkt Shein.
Ameongeza kuwa kwa umuhimu huohuo, na kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na kuyapa nguvu masuala ya Diaspora kilianzishwa kitengo cha Diapora na baadae idara ya Diaspora ilinzishwa hapa Zanzibar. Ililitengenezwa sera maalumu ya wanadiaspora, na sasa tupo mbioni kuanzisha sheria ya Diaspora, rasimu ya sheria hiyo imefikia katika hatua nzuri.
“Kwa matiki hiyo basi, namuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Issa Haji Ussi Gavu kuhakikisha anasimamia kwa karibu sana utayarishaji na kukamilika kwa rasimu ya sheria hiyo na iwasilishwe kwenye Baraza la wawakilishi kabla ya mwezi mei 2020,” Amesema Dkt. Shein.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, George Simbachawene akitoa shukrani kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Shein amesema kuwa sera ya Diaspora kwa upande wa Tanzania rasimu ya kwanza tayari imekamilika na hatua inayofuata ni kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wanadiaspora wenyewe kupitia balozi zetu ili na wao waweze kutoa mawazo yao.
“Mhe. Rais, kwa sasa sera ipo katika hatua nzuri, jitihada kubwa zinaendelea na jambo hili linahitaji kushughulikiwa kwa uangalifu mkubwa kwa sababu ya historia ya nchi yetu,” Amesema Simbachawene.
Aidha, Waziri Simbachawene aliongeza kuwa ni muhimu kutumia wanadiaspora kama fursa, sekta muhimu katika ujenzi wa uchumi wa taifa letu na mataifa mengi dunini yanafanya hivyo
Awali akitoa salamu za wanadiaspora, Mwenyekiti wa wanadiaspora, Norman Jasson alisema kuwa Sera ya Diaspora ina umuhimu wa kipekee kwani wanaamini kuwa sera hiyo itakapokamilika itatoa majibu ya maswali mengi ambayo yamekuwa yakiwanyima usingizi.
“Tunaamini sera hii itasaidia sio tu masuala ya uraia wa nchi mbili au hadhi maalum, bali pia masuala mengine kama umiliki wa ardhi, mirathi, ndoa kwa wenyeji na wageni, ruhusa ya makazi nchini kupitia vibali au visa na mengine mengi”
Ambapo amesema wanadiaspora wanaamini kuwa sera hiyo itarahisisha utungaji wa sheria itakayowatambua watanzania wote walio ughaibuni bila kujali kama tayari wameshachukua uraia wa nchi nyingine au kama tayari wana vibali vya makazi katika nchi wanazoishi na pia bila kujali waliingiaje ughaibuni katika kusaka maisha.