Siku moja baada ya wenyeviti wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kumkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt Wilbroad Slaa ameyatoa ya moyoni.

Kupitia akaunti yake Twitter leo mchana, Dkt Slaa alitumia tweets kadhaa kutoa majibu ya sintofahamu iliyojitokeza baada ya tukio la Edward Lowassa kuonekana akihudhuria kikao cha kamati kuu ya chama hicho usiku wa kuamkia jana.

Mpangilio wa tweets za Dkt Slaa zinazoelezea kwa kina suala hilo na kusisitiza kuwa Edward Lowassa bado ni mwanachama wa CCM, na kwamba hajajiunga na Chadema kama wengi wanavyoeleza huku akiwatupia mpira Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Huu ni mfululizo wa tweets za Dr. Slaa:

“1. Usiku wa kuamkia Julai 27 Chadema tulifanya kikao cha Kamati Kuu jijini Dar es Salaam, Kikao maalum cha Chama na ajenga za Uchaguzi Mkuu.”

“2. Kikao huwa na mlolongo wa mijadala na ni kawaida kwa vyama kualika watu mbalimbali katika baadhi ya mijadala yao kutegemea unyeti wake.”

“3. Moja ya wageni waalikwa alikuwa Edward Lowassa. Alialikwa kwa mambo ambayo yataainishwa hapa. Kisha tutaendela na dondoo za Kikao.”

“4. Lowassa amealikwa kama kiongozi toka CCM, na amealikwa kwa kuomba kwake mwenyewe kuhudhuria sehemu tu ya mjadala wa chama.”

“5. Kama kama mmoja ya wanasiasa wenye ushawishi na ambaye amekuwa na tuhuma nyingi ametueleza kwa kina zaidi mengi ambayo umma haukufahamu.”

“6. Si muda wa kuzungumza undani wa mazungumzo yake na Chadema, muda huo utafika na yote yatawekwa bayana kwa Watanzania wote.”

“7. Kwa miaka 23 upinzani sasa umefikia hatua ya kuongoza nchi yetu. Watanzania watambue kwamba tuko makini sana katika wakati huu.”

“8. Tuna intelijensia ya kutosha kujua nini kinaendelea, nani anahama CCM na kwa nini, nani anakuja kwetu kwa mema na nani ametumwa.”

“9. Muda wa Chadema kuchukua makapi, kuyumbishwa na intelijensia butu ya nchi ulipita zamani. Chama tawala kinatambua hili kwa wazi kabisa.”

“10. Tunaomba iwepo subira, tunakaribisha wana CCM wanaotaka kuja kujieleza mbele yetu, tutawajadili tutaripoti kwa Watanzania, tutaamua.”

“11. Wako wana CCM ambao wamekuja kwetu kujieleza kuhusu tuhuma zao na vielelezo lukuki, Lowassa si wa kwanza wala wa mwisho kufanya hivyo.”

“12. Ukituhumiwa, ukajieleza na kutupa vielelezo visivyo na shaka vya nani hasa mwenye kosa tutakusikiliza, Watanzania watakusikiliza.”

“Ndugu Watanzania, CCM ni kansa. Imekula nchi, imeongopa, imeua, haina dira. Sii CCM ya Mwalimu. Tatizo namba 1 la Watanzania ni CCM.”

“Kwa miaka 10 tumekwama katika kundi la nchi masikini zaidi duniani.

Bado sisi ni moja ya nchi ambazo wananchi hawana Bima ya Afya ya umma.”

“Kwa miaka 10 tumeona elimu yetu ikiporomoka mbele ya macho yetu huku shilingi ikifa mbele ya sarafu za kigeni. Si bahati mbaya, ni mfumo.”

“Kwa vijana: nina matumaini makubwa sana na ninyi. Uchaguzi huu wa 2015 fikiri kuhusu hatima ya nchi hii na ushiriki wako. Fikiria uzao wako.”

“Wana-CCM popote walipo wasidhani kwamba wakishindwa walipo watakuja Chadema na moja kwa moja tutawapa nafasi. Tuna utaratibu, tutaufuata.”

“Mpaka sasa Lowassa ni mwana-CCM, ana kadi ya CCM. Sio mwana Chadema, wala mgombea wa Chadema. Propaganda zinaenezwa na CCM, waulizwe wao.”

Bayern Munich Washtukia Mchezo Wa Man City
Rais Putin Amsafisha Sepp Blatter