Siku kadhaa baada ya vyombo mbalimbali vya habari kuripoti habari kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt Wilbroad Slaa amejiondoa katika chama hicho baada ya Edward Lowassa kupewa nafasi ya kuwania urais, amejibu tetesi hizo kwa mara ya kwanza.

Slaa ambaye ukimya wake na kutoonekana kwake kwenye mikutano ya Chadema baada ya Lowassa kukabidhiwa kadi ya chama hicho, alizungumza na waandishi wa habari wa gazeti la Mtanzania kwa njia ya simu na kukanusha tetesi hizo.

Tetesi hizo za kujitoa Chadema ziliambatana na tetesi nyingine kuwa mkewe, Josephine Mushumbusi kuwa ndiye anaemkataza kuendelea na chama chake na kwamba amemfungia ndani ili asihudhurie matukio ya chama hicho.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, jana waandishi wake walifika nyumbani kwa Dkt. Slaa eneo la Mbweni, Dar es Salaam  na kumkuta mlinzi ambaye aliwaeleza kuwa waliyemtafuta hayupo muda huo.

Waandishi hao waliamua kumpigia simu mke wa Dkt Slaa ambaye licha ya kukiri kuwa wapo wote muda huo, alikanusha vikali tetesi hizo.

“Mnatakiwa kuwa na akili mnasikia eeeh! Yaani nimfungie Dkt kwani yeye amekuwa mtoto mdogo?” Josephine alikaririwa.

Dkt Slaa aliamua  kuongea na simu hiyo baada ya kusikia maongezi ya mkewe na baada ya kuulizwa tetesi za kujiengua Chadema na kufungiwa ndani na mkewe alikanusha kwa mshangao.

“Hivi mwandishi mkubwa unaweza kufuatilia habari hizi? Hivi sasa mimi nipo Sabasaba mbele ya polisi nikiendesha, hivi hiyo nyumba hapa iko wapi, na nani anifungie na kwanini?” aliuliza Dkt Slaa na kuongeza kuwa mtu anayetakiwa kujibu taarifa hiyo ni aliyeitoa.

Jana, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu ambaye alijitokeza wakati wa Edward Lowassa anachukua fomu za kuwania urais kupitia chama hicho baada ya tetesi za muda mrefu kuwa naye amejitoa, alisema kuwa viongozi wote wa chama hicho walishiriki katika hatua za kujadili hadi kumpitisha Lowassa.

 

 

 

Lowassa: Tutashinda Bila Kashfa Na Matusi
Maradona Atangaza Vita Na Vimelea Vya Rushwa