Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax amekutana na kuwaaga mabalozi watatu waliokuwa wanaziwakilisha nchi zao hapa nchini baada ya kumaliza muda wao wa uwakilishi.

Dkt. Tax amewaaga mabalozi hao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambao ni Balozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya nchini, Manfredo Fanti, Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess pamoja na Balozi wa Norway Nchini, Elisabeth Jacobsen.

Awali Tax alimpongeza Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini, Fanti kwa ushirikiano alioutoa kwa Serikali ya Tanzania wakati wa uwakilishi wake na kumuahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya wakati wote hususani katika sekta ya biashara na uwekezaji.

Amesema, “tumekuwa na makongamano kadhaa ya biashara yaliyowakutanisha wafanyabishara wa mataifa yetu na kujadili fursa za biashara baina ya mataifa yetu,” huku Balozi Fanti akiishukuru Tanzania kwa ushirikiano iliompatia wakati wote wa uwakilishi na kuahidi kuwa ataendelea kuwa Balozi bora wa Tanzania.

Aidha, Dkt. Tax amemuaga Balozi wa Ujerumani nchini hapa nchini, Regine Hess na kumshukuru kwa ushirikiano aliouonesha kwa Serikali ya Tanzania wakati wa uwakilishi wake hapa nchini kwa kusema “tunakushukuru kwa ushirikiano wako wakati wote wa uwakilishi wako hapa nchini, ushirikiano wetu (Tanzania na Ujerumani) umekuwa imara na bora wakati wote na tunaamini utaendelea kuimarika,” alisema Dkt. Tax.

Naye Balozi Hess alisema kuwa anaondoka akiwa na faraja ya kuona masuala ya utawala bora, haki za binadamu pamoja na amani na usalama yakiwa yameboreshwa kwa kiasi kikubwa ambapo pia Dkt. Tax amekutana na kumuaga Balozi wa Norway nchini, Elisabeth Jacobsen aliyeishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano wakati wa kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.

Rais Mwinyi ateta na Katibu wa Bunge Ujerumani
Rais mgeni rasmi maadhimisho kupinga dawa za kulevya