Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muugano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson Mwansasu amechukua fomu za kuwania kiti cha spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hii leo Januari 10, 2022 katika ofisi ndogo za Chama cha Mapinduzi Lumumba Dar es salaam.
Tayari aliyekuwa Mbunge wa Shinyanga Mjini na Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele ameshachukua fomu ya kugombea Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hapo jana Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitangaza kuanza mchakato wa kumsaka mrithi wa nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ambaye alijiuzulu tarehe 6 Januari mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Visiwani Zanzibar, Katibu wa NEC- Itikadi Uenezi CCM, Shaka Hamidu Shaka amesema mchakato huo utaanza kuanzia tarehe 10 hadi 30 Januari mwaka huu.
Hatua hiyo imekuja baada ya Job Ndugai kuandika barua kwa hiari yake ya kuachia nafasi hiyo na kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa CCM jijini Dodoma.