Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM), Dk Tulia Akson amechaguliwa kuwa Spika mpya wa Bunge la Tanzania akichukua nafasi iliyoachwa na Job Ndugai aliyejiuzulu nafasi hiyo Januari 6, 2022.
Uchaguzi huo umefanyika leo Jumanne Februari Mosi 2022 Bungeni jijini Dodoma ukiongozwa na Mwenyekiti wa uchaguzi, Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi.
Akitangaza matokeo hayo, Lukuvi amesema Dkt. Tulia ambaye alikuwa akichuana na wagombea wengine nane ameshinda kwa asilimia 100 akijizolea kura zote 376.
“Dkt. Tulia Ackson huyu ni mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amepata kura zote 376,” amesema Lukuvi huku wabunge wakishangilia.
Lukuvi amesema wapiga kura walikuwa wabunge 376 na hakuna kura iliyoharibika huku wagombea wengine wote nane wakiwa hawajapata kura.
Baada ya kuchaguliwa, Dk Tulia alikula kiapo na baadaye kutoka nje ya ukumbi kuvaa vazi la Spika na kurejea ndani kuendesha kikao cha Bunge.
Kabla ya kuanza kuendesha kikao chake cha kwanza akiwa Spika, Dk Tulia alianza kumuapisha Mbunge mpya wa Ngorongoro, Emmanuel Shanghai.
Katika utumishi wake wa unaibu Spika, Tulia alipata pia uzoefu mwingine ambao pengine hakuna mtangulizi wake mwingine alipata kuwa nao. Kuna jambo moja lisilo la kawaida lilitokea lililompa Tulia jambo ambalo manaibu Spika waliomtangulia hawakulipata.
Jambo hilo lilikuwa ni kuugua kwa Ndugai. Miezi michache tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Ndugai alipata changamoto za kiafya zilizosababisha aende kutibiwa nje ya nchi alikokaa kwa takribani miezi sita. Changamoto hiyo ilisababisha Tulia aanze kufanya kazi ambazo kwa kawaida Spika huwa hamwachii naibu wake azifanye.
Kwa kifupi, katika wakati wa ugonjwa wa Ndugai, Tulia alikuwa kama Spika kamili asiye na cheo tu cha kuthibitishwa. Kuna historia ya migongano ya kikazi kati ya Spika na Naibu katika Bunge la Tanzania lakini Tulia – katika bahati ya peke yake, hakuwa nayo katika miezi yake ya kwanza kwenye cheo hicho kwa sababu bosi wake hakuwepo.
Tulia alizaliwa katika Kijiji cha Bulyaga, wilayani Tukuyu mkoani Mbeya mnamo Novemba 23 mwaka 1976. Ni mhitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika sheria kutoka katika Chuo Kikuu mashuhuri cha Cape Town, Afrika Kusini.
Alianza elimu yake ya Msingi katika Shule ya Mabonde na kupata elimu ya awali ya sekondari kwenye shule ya Loleza iliyopo Mbeya. Kwa masomo ya sekondari ya juu, Tulia alisoma katika Shule ya Zanaki jijini Dar es Salaam.
Aliajiriwa na UDSM mwaka 2001 kama mhadhiri msaidizi mara baada ya kumaliza masomo yake ya shahada ya kwanza na ya pili ambapo alikuwa mmoja wa wanafunzi bora katika kitivo cha sheria.
Tulia ameolewa, mumewe anaitwa James Mwainyekule.