Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kundi la Afrika katika Umoja wa Mabunge Duniani (Africa Geopolitical Group in the IPU), Dkt. Tulia Ackson, amehutubia Mkutano wa 146 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaoendelea Nchini Bahrain.
Katika mkutano huo, Dkt. Tulia amezungumzia kuhusu kuhusu juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Bunge katika kudumisha amani na mahusiano mazuri ya kijamii kwa Wananchi wake pamoja na kuheshimu Maazimio ya Kimataifa katika kulinda na kudumisha amani Duniani.
Aidha, pia alitumia nafasi hiyo kuwasilisha hoja ya dharura kwa niaba ya kundi hilo kuchagiza kuundwa kwa mfuko wa maafa Duniani kwa ajili ya kusaidia Nchi zinazoathiriwa na majanga ya asili na mabadiliko ya tabianchi.
Hoja nyingine nne ziliwasilishwa na Mataifa mbalimbali na zinatarajiwa kupigiwa kura ya maamuzi hapo baadae ili Umoja huo kupitisha hoja moja ya dharura ambayo itajadiliwa, kuboreshwa na hatimaye kutengeneza azimio la Mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu isemayo, “Kukuza amani na kujenga Jamii Jumuishi yenye kuvumiliana”.