Fedha nyingi za Uviko 19 zilizoelekezwa katika kukarabati Sekta ya afya imewapunguzia mzigo wanawake hasa waliopo maeneo ya vijijini waliokuwa wakifuata huduma hiyo umbali mrefu.
Hayo yamesemwa na Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson leo Jumamosi Machi 19, 2022 wakati wa kongamano la tathmini ya mwaka mmoja wa Rais Samia tangu alipoapishwa rasmi kuwa Rais wa Tanzania Machi 19, 2021.
Amesema Rais Samia aliingia madarakani kipindi ambacho nchi inapitia wakati mgumu wa janga la Uviko-19 na alifanikiwa kupata mkopo kwa ajili ya kupigana na changamoto hiyo Sh13 trilioni zilizotoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambazo alizielekeza katika maeneo nyeti ikiwemo elimu na afya.
“Haya maeneo yote yanawagusa wanawake. Eneo la afya fedha hizo zilinunua magari ya wagonjwa ya kisasa 20 na ya kawaida 365, ujenzi vituo vya dharura na vifaa ngazi zote za halmashauri hadi taifa.
“Umefanyika uimarishaji wa mfumo wa usambazaji na ununuzi wa mitungi ya gesi, hospitali za rufaa na usimikaji wa vinu 44 vya hewa ya oksijeni hospitali za halmashauri mpaka taifa,” amesema.
“Hapa nitoe ufafanuzi zaidi, mkisikia wanampenda si sababu ni mwanamke mwenzao ila maeneo ambayo ameyafanyia kazi yamewapunguzia pakubwa sana mzigo ambao walikuwa wanaubeba, huduma za afya zikiwa zinapatikana mbali wanaopata tabu zaidi ni wanawake sababu wao ndiyo wahudumiaji wagonjwa,” amesema.
Amesema mwanamke anapokuwa na mgonjwa hospitalini kama yupo mbali atasafiri akalale huko auguze lakini kama zipo karibu hana haja ya kulala hospitali.
“Maeneo aliyoyagusa yanawapunguzia mzigo wanawake, ukianza kuchambua zaidi utagundua kwamba mlolongo unaenda mbali zaidi si kulala hospitali mambo mengi inabidi yasimame, atarudi kijijini na kurudi mjini saa ngapi mambo yote yanasimama,” amesema.
Spika amesema Rais Samia pia ametoa kiasi cha Sh137.3 bilioni kutekeleza elimu bure.