Wazazi wa Wanafunzi waliofariki katika shambulio lililofanywa na Waasi wa kikundi cha Allied Democratic Forces – ADF, katika Shule ya Sekondari ya Lhubiriha nchini Uganda, wamelazimika kuwasilisha sampuli za vinasaba (DNA), ili kuitambua miili ya watoto wao.
Wazazi hao, ni wale ambao hawajapata miili ya watoto wao katika maiti 42 zilizopatikana baada ya tukio la Juni 16, 2023 ambapo Washambuliaji walichoma moto bweni la wanafunzi wavulana, na baadaye kushambulia bweni la wasichana kisha kuwauwa kwa kuwakatakata kwa mapanga na visu.
Katika tukio hilo, pia washambuliaji hao waliwateka nyara wanafunzi sita huku Maafisa wa usalama wakisema ADF wana uhusiano na wapiganaji wa kundi la Islamic State – IS, lenye makao yake upande wa pili wa mpaka wa Uganda katika misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Tai Ramadhan alisema maiti nyingi zilichomwa moto kiasi cha kutoweza kutambulika, hivyo kuwalazimu wachunguzi kutumia sampuli za DNA kutoka kwa ndugu na jamaa ambao wanajaribu kuwatambua.