Uongozi wa timu ya Dodoma FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) umepanga kikosi chao kuanza mazoezi rasmi Mei 28 kujiandaa na mechi zao zilizosalia.
Kikosi hicho kinachonolewa na kocha Mbwana Makata kitaingia kambini Mei 27 ambapo wachezaji wote wanapaswa kuwepo kwa ajili ya mpango wa mazoezi ambao itawawezesha kujiimarisha zaidi kabla ya kuelekea Mwanza ambapo ndicho kituo kinachotumika kwa ajili ya mechi za FDL na Daraja la Pili (SDL).
Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji FC, Fortunatus John amesema kuwa, timu itaingia kambini ikiwa na matumaini makubwa na ari ya mazoezi kwa lengo la kuivusha timu hiyo kutoka FDL kuelekea Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) msimu ujao.
Amesema, pamoja na matumaini hayo lakini pia wanaangalia namna yakutatua changamoto ya bajeti yao ya ndani kwa kuzingatia kuwa ile ya awali ilikuwa inaishia Aprili 30, hivyo timu inamahitaji makubwa ya kifedha ambayo itasaidia kutekeleza majukumu ya kimsingi ndani ya kambi.
“Hadi Ligi inasimama, tulikuwa kileleni mwa kundi A tukiwa na pointi 39 tukiwaacha alama mbili Ihefu wenye pointi 37 hivyo tunaingia kambini tukiwa na ari kubwa katika michezo yetu iliyobaki na tumedhamiria kurejesha furaha ya soka hapa Dodoma na kupanda Ligi Kuu ambapo kwa muda mrefu hatukua na timu inayoshiriki Ligi hiyo,” amesema Katibu huyo.
Kwa upande wao Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Hamisi Kisoy wametoa pongezi kwa Serikali kwa kuruhusu kuendelea kwa Ligi za Soka huku akiitaka Dodoma FC, JKT Tanzania, Area C United, na nyingine kuanza mazoezi ili kujiweka sawa kuelekeakwenye mechi zao zilizosalia huku wakizingatia maelekezo kutoka Wizara ya Afya.
“DOREFA tumejipanga kutoa kila aina ya ushauri wa kiufundi ili kuhakikisha timu zetu zinafanya vizuri katika Ligi husika, lakini pia naomba wadau wa soka kuzisaidia kwa hali na mali timu hizi ili kufikia malengo yao,” amesema Kisoy.