Uongozi wa klabu ya Dodoma Jiji FC umetamba timu yao haitokuwa tayari kufungwa mara mbili dhidi ya vinara wa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC.

Tambo hizo za uongozi wa Dodoma Jiji FC ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Msimu huu wa 2020/21 zimetolewa, huku kikosi cha klabu hiyo kikitarajia kuwa mgeni wa Simba SC, leo Jumanne (April 27) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salam, kuanzia mishale ya saa moja jioni.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Dodoma Jiji FC, Moses Mpunga amesema kikosi chao kimejiandaa kikamilifu kuelekea mchezo huo, na wana uhakika wa kupata alama tatu muhimu mbele ya Simba SC, licha ya kuwa timu tishio katika Ligi Kuu msimu huu.

“Mchezo wa leo ni mchezo wa mabingwa. Dodoma Jiji ni Mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza na Simba ni Mabingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita. Wana medali ya dhahabu na sisi tuna medali ya dhahabu. Wana kocha bora na sisi tuna kocha bora. Wana mchezaji bora msimu uliopita na sisi tuna mchezaji bora wa ligi daraja la kwanza.”

“Kwa hiyo utakuwa mchezo wa mabingwa, utakuwa mchezo nzuri. Watu wajitokeze kwa wingi, tunakwenda kuwashangaza Watanzania. Sisi huwa hatufungwi mara mbili,” amesema Mpunga.

Mchezo wa mzunguuko wa kwanza Dodoma Jiji FC wakiwa nyumbani Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, walikubali kufungwa mabao mawili kwa moja dhidi ya Simba SC, mabao yakifungwa na washambuliaji Bernard Morrison na Meddie Kagere , huku bao la wenyeji likifungwa na Cleoface Mukandara.  

Dodoma Jiji FC kwa sasa ipo katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 38, huku Simba SC wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha alama 58.

Mangungu azikatisha tamaa Young Africans, Azam FC
ASFC: Young Africans waifuata Tanzania Prisons