Kocha wa Dodoma Jiji FC Masoud Djuma Irambona amesema kikosi chake bado kina nafasi ya kupambana ili kufikia lengo la kumaliza kwenye nafasi nne za juu msimu huu 2021/22.

Masoud Djuma ameonesha matumaini hayo, baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Biashara United Mara jana Alhamis (Mei 05), katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema nafasi ya tatu na nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu bado zipo wazi, na dhamira yake ni kuhakikisha Dodoma Jiji FC inakuwa sehemu ya nafasi hizo.

Amesema ni vigumu kwa sasa kuifikia nafasi ya kwanza ama ya pili, kutokana na Manguli wa Soka la Bongo (Young Africans na Simba SC) kujizatiti kwenye nafasi hizo, hivyo nafasi iliyobaki ni kupambana ili kumaliza nafasi ya tatu ama ya nne.

“Simba SC na Young Africans zimeshatangulia, nafasi ya tatu na nne bado zipo wazi, ni jukumu letu kuendelea kupambana ili kuzifikia nafasi hizo, naimani kila kitu kinawezekana.”

“Kupata alama tatu katika uwanja wa ugenini tena kwa kuifinga timu ngumu Biashara United Mara, inafaa kujipongeza na kufikiria namna ya kusonga mbele, bado nina matumaini tutafanikisha dhamira yetu.”

“Ukishaondoka katika mstari mwekundu wa kushuka daraja, unapaswa kufikiria namna ya kwenda juu zaidi, hasa katika Ligi hii timu zimekaribiana sana kwa alama, kwa hiyo sina wasiwasi, tutaendelea kupambana hadi mwisho.” amesema Kocha Masoud Djuma Irambona

Dodoma Jiji FC imefikisha alama 27 zinazoiweka katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku timu za Namungo FC na Azam FC zinazoshika nafasi ya tatu na nne zikiwa na alama 30 kwa 29.

Biashara United Mara imesalia nafasi ya 12 ikiwa na alama 23, ambazo zinaifanya kuwa na tofauti ya alama mbili dhidi ya Coastal Union inayoburuza mkia kwa kuwa na alama 21.

Haji Manara: Hatutarudia makosa
Wachezaji Mbeya Kwanza FC wapongezwa