Kikosi cha Dodoma Jiji FC kinaendelea kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Geita Gold FC ambayo itakua nyumbani katika Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita, mwanzoni mwa juma lijalo.
Dodoma Jiji FC inayonolea na Kocha kutoka nchini Burundi Masoud Djuma Irambona, imeweka kambi mjini Dodoma ikijiandaa na mchezo huo, ambao wanaupa umuhimu mkubwa kutokana na hatari ya kushuka daraja inayowakabili.
Kocha Masoud Djuma amesema anatambua mchezo dhidi ya Geita Gold utakua na upinzani mkubwa na kibaya Zaidi watakua ugenini, hivyo anautumia muda huu kujiandaa, ili kuwawezesha wachezaji wake kutambua mbinu atakazozitumia kwenye mchezo huo.
“Geita Gold ni timu nzuri, ina kocha mzuri, na wapo katika nafasi nzuri tofauti na sisi, halafu ni vigumu sana kuwafunga wakiwa kwao, kwa hiyo tuna kazi kubwa ya kufanya katika mchezo huo.”
“Ninasikia wanacheza vizuri, mimi sijabahatika kuwaona wakicheza, hii ni mara ya kwanza kukutana na Geita Gold, ninaamini itakua kazi ngumu sana kwa sababu siwatambui kama nilivyobahatika kuwatambua wengine niliowahi kucheza nao tangu nilipoanza kazi hapa,”
“Tunajipanga kwa kufanya maandalzii mazuri, wachezaji wangu wapo katika hali nzuri na wanaendelea kudhihirisha hilo katika mazoezi yetu ya kila siku hapa Dodoma, kwa hiyo ninaamini watapambana na timu yenye uwezo mkubwa, na wao wanajua cha kwenda kufanya huko Geita.” Amesema Kocha Masoud
Dodoma Jiji FC ipo nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 31, huku Geita Gold FC ikishika nafasi ya 05 kwa kufikisha alama 36.