Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali imetenga kiasi cha dola za kimarekani bilioni 4.7 kwa ajili ya kuwezesha mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wataalamu wa TEHAMA nchini.

Takwimu hiyo imetolewa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Khamis Abdulla katika hafla ya kuwakabidhi vyeti vya ufadhili wa masomo ya muda mrefu nje ya nchi watumishi wa umma wapatao 20 kutoka katika Wizara, taasisi za umma na halmashauri za miji na wilaya.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla akizungumza wakati wa hafla ya kuwakabidhi vyeti vya ufadhili wa masomo ya muda mrefu nje ya nchi kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali awamu ya kwanza iliyofanyika leo jijini Dodoma.

Amesema, “nitoe rai kwa kila aliyepata ufadhili huu, kutumia kikamilifu fursa hii kujifunza kwa bidii kwa lengo la kuongeza uelewa na maarifa ili mtakaporudi muweze kuleta mabadiliko chanya yatakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma za Serikali.”

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema kuwa watumishi hao wanakwenda kuongeza ujuzi na maarifa na watakaporejea ofisi hiyo itahakikisha wanatumika vizuri kitaifa na kimataifa.

Picha wakati wa hafla ya kuwakabidhi vyeti vya ufadhili wa masomo ya muda mrefu nje ya nchi kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali awamu ya kwanza iliyofanyika leo jijini Dodoma.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Gerald Mbwafu amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatambulika katika balozi za Tanzania lakini pia kuwa wazalendo na kuiwakilisha nchi vizuri.

Awali Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya, Bi. Salome Kessy akitoa taarifa ya ufadhili huo amesema Mradi wa Tanzania ya kidijitali umepanga kutoa ufadhili wa mafunzo kwa watumishi 500 kati ya hao watumishi 50 watapatiwa mafunzo ya muda mrefu na watumishi 450 watapatiwa mafunzo ya muda mfupi katika maeneo ya teknolojia zinazoibukia.

OSHA yatoa uelewa utekelezaji wa majukumu yake
Tuhuma za Mikutano: Lissu, Mbowe watoa kauli