Kiungo wa Liverpool, Dominik Szoboszlai amedai atafanya juu chini kutimiza ndoto za kubeba mataji msimu huu na kuipiku Manchester City ambayo ndio mabingwa watetezi.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22 alionyesha kiwango safi katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu England dhidi ya Bournemouth baada ya uhamisho wa Pauni 60 milioni.

Akizungumza kupitia ukurasa wa Liverpool Echo, kiungo huyo alisema: “Tutaona. Tuna mechi nyingi za kucheza kama Man City ambao pia tutacheza nao. Kila timu ina nafasi ya kushinda.

“Hata sisi mawazo yetu ni kupata matokeo mazuri, mimi ndio nilivyo, napenda kushinda, napenda kufanya kila kitu kwa ajili ya timu kama nataka kubeba Europa au Kombe la FA, tunaweza kufanya makubwa mwaka huu.” Alisema Szoboszlai.

Kiungo huyo pia alizungumzia urafiki wake na straika wa Man City Erling Haaland akidai nyumba zao wanazoishi zinafuatana.

“Anaishi karibu na nyumba yangu, nyumba zetu zinafuatana. Tulikuwa tunawasiliana, kuna wakati tunafanya mazoezi pamoja,” aliongeza kiungo huyo ambaye amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Liverpool baada ya kuleta uhai katika safu ya kiungo.

Katika misimu yake sita aliyocheza, alibeba makombe tisa na hivi karibuni alinyakua Kombe la Ligi akiwa na RB Leipzig kabla ya kutua Anfield.

Katika fainali waliyocheza dhidi ya Eintracht Frankfurt kiungo huyo alifunga bao katika ushindi wa mabao 2-0 na sasa ameweka wazi anataka kupata mafanikio Anfield.

Azam FC kujiuliza tena leo
Waziri asimamishwa kazi kwa usaliti