Hatimae mlinda mlango wa kutumainiwa wa klabu ya AC Milan Gianluigi Donnarumma, amekubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo inayocheza ligikuu ya soka nchini Italia, Serie A.
Mlinda mlango huyo mwenye umri miaka 18, amefikia maamuzi ya kukubali kusaini mkataba mpya, baada ya kusitisha mpango wake wa kugoma kufanya hivyo.
Mkataba mpya wa mlinda mlango huyo, utampa fursa ya kuendelea kubaki klabuni hapo hadi mwaka 2021, na pia unavunja tetesi za kutaka kuhamia kwenye klabu za Real Madrid na Manchester United, ambazo zilikua zinatajwa kumuwania katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.
Mkataba wa sasa wa Donnarumma ulikuwa unafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.
-
Novak Djokovic atinga robo fainali Wimbledon
-
James Rodriguez atimkia Bayern Munich kwa mkopo
-
Arsene Wenger: Tutasajili Wachezaji Wenye Hadhi Kubwa
Donnarumma amekuwa na kiwango kizuri cha kulinda lango, hali ambayo imemuwezesha kuitumikia timu ya taifa ya Italia chini ya umri wa miaka 21 tangu mwaka 2015, kabla ya kuitwa kwenye kikosi cha wakubwa mwaka 2016 ambapo amecheza michezo minne hadi sasa.
Mwezi uliopita, Donnarumma alirejeshwa katika kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 21 na alicheza katika fainali za Ulaya zilizounguruma nchini Poland.
Akiwa katika fainali hizo mashabiki waliosadikiwa kuwa ni wa AC Milan walionyesha hasira dhidi yake, na kufikia hatua ya kumrushia fedha bandia akiwa langoni kwake, ikiwa ishara ya kumfikishia ujumbe wa kuisaliti klabu yao.
Hatua hiyo ilichukuliwa na mashabiki hao, baada ya kuchukizwa na hatua ya Donnarumma ya kukataa kusaini mkataba mpya.