Wakati wadau na mashabiki wa soka wakijiuliza hatima ya beki Mamadou Doumbia ndani ya Young Africans kutokana na kutoonekana kikosini pia akiwa hajapewa Thank You’ kama ilivyotokea kwa wengine, Taarifa za kuaminika zinaeleza kuwa hawajamalizana.
Young Africans ilimsaini Doumbia katika dirisha dogo la msimu uliopita sambamba na kiungo Mudathir Yahya na mshambuliaji Kennedy Musonda ambao wanaendelea kukiwasha, lakini beki huyo raia wa Mali haonekani kikosini.
Baada ya Young Africans kufanya siri na baadhi ya viongozi kuulizwa na kushindwa kuweka wazi juu ya Doumbia aliyesaini mkataba wa miaka miwili, mmoja ya vigogo wa timu hiyo, amefunguka kuwa bado hawajamalizana, lakini wapo kwenye hatua nzuri na siku sio nyingi wataafikiana.
Chanzo hicho kimesema hatua iliyopo ni kumtafutia timu ili kumuuza ama kumtoa kwa mkopo na wako mbioni kukamilisha hilo.
“Bado tunatafuta njia nzuri ya kulimaliza hili. Kila upande umeafiki tulichokiamua na sasa kwa kushirikiana na uongozi wa mchezaji, tupo kwenye hatua za mwisho za kumpatia timu atakayocheza msimu ujao na hapo kuna mawili, kumuuza au kumtoa kwa mkopo,” kimesema chanzo hicho.
Kilichotokea kwa Doumbia ni kama kilichotokea kwa Gael Bigirimana aliyesajiliwa na Young Africans msimu uliopita, lakini akatemwa dirisha dogo na kushindwa kuafikiana kiasi cha hivi karibuni kurejea kikosini kimyakimya au ilivyo kwa Peter Banda wa Simba SC inayeelezwa amempisha kipa Ayoub Lakred, huku akiwa bado yupo kikosini akisikilizia hatima ya kutafutiwa timu iwe kwa mkopo au kuuzwa.