Nchini Kenya Naibu Rais William Ruto ameahidi kuwa atamrejesha nyumbani wakili aliyefukuzwa nchini humo Miguna Miguna iwapo atashinda uchaguzi wa urais mnamo Agosti 9, 2022.
Licha ya Mahakama Kuu Nchini humo kusema kuwa alifukuzwa kinyume na sheria bado jaribio la kurejea Kenya limekuwa likikumbwa na kizingiti.
Akizungumza na Sauti ya Amerika Ruto amesema jaribio la Miguna kurejea Kenya limekuwa gumu Miguna tangu alipotimuliwa nchini mwaka 2018 licha ya Mahakama Kuu kuamua kuwa alifurushwa kinyume cha sheria.
Ruto alisema atamruhusu wakili huyo kurejea nchini punde tu atakapokuwa rais kwa sababu, licha ya yotee, Miguna ni raia mzaliwa wa Kenya ambaye anastahili kuwa nyumbani.
“Nitamrudisha nyumbani mara moja! Yeye ni Mkenya na hajafanya lolote baya. Ikiwa amefanya lolote, arudishwe nyumbani na kukabiliana na sheria nyumbani.” “Si busara kwamba tunakaribisha watu waliohamishwa nchini Kenya ilhali mmoja wetu yuko Canada,” amesema Ruto
Kupitia mtandao wa kijamii, Miguna aliandika kuwa ”Ruto akisema alijibu vyema maswali aliyoulizwa kwenye mahojiano. “Swali zuri, ambalo William Samoei Ruto alijibu kwa usahihi. Lakini lazima aende mbali zaidi: kulaani ukiukaji wa haki za binadamu, ukiukaji wa katiba na kutotii amri za mahakama,” alisema.
Mpaka sasa imesalia miezi 6 kabla ya uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 9 2022, huku wagombea wa kiti cha Urais wakiendelea kutoa sera kwa wananchi katika kipindi hiki cha kamapeni.