Naibu Rais William Ruto ametangaza hadharani nia yake ya kukabiliana na ufisadi iwapo atachaguliwa kuwa rais baada ya mwezi Agosti mwaka huu ambapo nchi hiyo inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu.
Ruto amesema kuwa changamoto iliyopo kwa sasa katika kukabiliana na ufisadi, inatokana na ofisi ya rais kuingililia idara ya Mahakama.
Ruto amefafanua kuwa ofisi ya rais imekuwa ikihitilafiana na idara ya mahakama kwa kushindwa kuitengea fedha za kutosha za kuendeleza shughuli zao.
“Nimejitolea kutenga hazina ya idara ya mahakama ili iwe na uhuru wa kutekeleza majukumu yake. Hatua hiyo itasaidia sana kuhakikisha kesi za ufisadi hazichukui zaidi ya miaka kwa idara ya mahakama, kushindwa kufuatia kupungukiwa na rasilmali ya kuwaajiri wafanyakazi zaidi ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” amesema Ruto.
“Kwa sasa, utahitajika kuapa kuunga mkono handshake au BBI, ili uondolewe mashtaka ya ufisadi. Sisi tunaamini kuwa sheria inapaswa kutekelezwa na idara zilizochaguliwa kikatiba katika kuwaadhibu washukiwa,” Ruto amesema.
Aidha amesema kuwa atahakikisha kwamba akiwa rais, ofisi yake haitaingililia kazi ya huduma za polisi au idara ya upelelezi wa jinai katika kutekeleza majukumu zikiwa huru.
Pia amesema kwamba ili kufanikisha mambo haya, atahakikisha idara husika zinapata fedha za kutosha, pasi kutegemea ofisi ya rais.