Abel Paul wa Jeshi la Polisi – Dar es Salaam.
Kituo cha Utafiti cha Jeshi la Polisi kilichopo Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam kwa kushirikina na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru – TICD, imeendelea na mafunzo awamu ya Pili kwa kundi la wanafunzi wa kozi ya Uofisa, yanayolenga kuwajengea uwezo na maarifa mapya katika kupambana na ukatili wa kijinsia.
Mkuu wa kitengo cha utatifi cha Jeshi la Polisi, Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam – DPA, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP. Ralph Meela ameyasema hayo na kudai kuwa kazi kubwa ya kituo hicho ni kufanya tafiti na kushirikiana na Taasisi za Elimu ya juu, ili kuwaongezea uwezo Maafisa na Askari wa Jeshi hilo.
Amesema, tayari zaidi ya Taasisi kumi zimeshafika chuoni hapo kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa Maafisa Wanafunzi na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi, huku akimshuru Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Camillus Wambura kwa kuwaunganisha na Taasisi za elimu ya Juu kufanya maboresha ya utendaji kazi unaoendana na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia.
Kwa upande wake Mhadhiri Msadizi kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Elinami Nassari amesema ni muhimu Jeshi la Polisi kuielewa jamii wanayokwenda kuihudumia, huku akiwaomba Maafisa hao Wanafunzi kufahamu mila na tamaduni husika, ili kutengeneza ushirikishwaji wa Jamii kikamilifu.
Kwa upande wake Mwanafunzi wa kozi ya Uofisa, Rose Mbaga amesema mafunzo hayo kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, yamewaongezea uwezo na maarifa mapya katika mapambano dhidi ya ukatili ya kijinsia.
Naye, Mwanafunzi wa kozi ya Uofisa, Issa Asali amewaomba wanafunzi wenzake kwenda kutumia njia rafiki walizofundishwa na Wahadhiri, pamoja na wawezeshaji kutoka Taasisi ya maendeleo ya Jamii Tengeru.