Mkurugenzi wa mashitaka DPP kutoka upande wa Jamhuri hii leo March 4, 2022 amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi dhidi ya Freeman Mbowe.
Mbowe na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya Ugaidi na leo walitakiwa kuanza kujitetea.
“Taarifa hii tunaiwasilisha kwa njia ya maandishi, kwa maombi hayo ya Kifungu cha 91(1) tunaomba kuondoa mashitaka yote dhidi ya washitakiwa wote sababu zote zipo katika Noel Prosecui ambayo tumeiwasilisha” alisema wakili wa serikali mbele ya jaji Joachim Tiganga ambaye amekua akisimamia kesi hiyo.
Baada ya Mahakama kusikiliza hoja iliyoletwa na wakili mwandamizi wa Serikali kwamba Mkurugenzi wa Mashitaka hana nia ya kuendelea na kesi hii, na upande wa pili wakaridhia, Mahakama inasema shauri hili lililokuwa linawakabili washitakiwa Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe linaondoshwa mahakamani na washitakiwa wanaachiwa huru bila masharti.
“Kwa sababu kuna vielelezo vililetwa Mahakamani, naandaa amri ya kuviachia, na hivyo naelekeza Mkuu wa Magereza kuwaachiwa mara moja leo na si vinginevyo.”
Freeman Mbowe alikamatwa na polisi yeye pamoja na wanachama wengine 10 wa CHADEMA mjini Mwanza wakati walipokuwa wakijiandaa kushiriki kwenye kongamano la kushinikiza kupatikana kwa katiba mpya mwezi Julai 2021 na wakati huo wote wamekua mahabusu huku kesi yao ikisikilizwa mahakamani.