Mkurugenzi wa mashtaka nchini DPP Biswalo Mganga amesema ni kosa kuwarejeshea fedha watu waliojiunga na kampuni ya Qnet kisha kudai kwamba wametapeliwa kwa kuwa biashara inayofanywa na kampuni hiyo ni upatu haramu.

DPP ameeleza hayo kufuatia Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini TAKUKURU mkoani Geita kurejesha shilingi Milioni 5.48 kwa mwalimu Rose Mgamba wa shule ya msingi Lukaranga aliyedai kutapeliwa.

“Sitaki kuona taasisi yoyote inawarudishia fedha wanaojiita waathirika wa biashara ya upatu, kama mwalimu au wakili yoyote wa serikali alicheza, amecheza mwenyewe kwa faida na hasara yake, hivyo sitaki kuona taasisi yoyote inawarudishia fedha watu waliocheza upatu kwa faida zao wenyewe,”amesema DPP.

DPP ameeleza kuwa shughuli inayofanywa na kampuni ya Qnet ni upatu haramu na tayari Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI ameanza upelelezi kuhusiana na sakata hilo na amezitaka taasisi zote zinazohusika na uchunguzi wa sakata hilo kushirikiana kwa kuwa wanajenga moja.

Aidha DPP amewaonya wananchi kuacha kucheza au kujiingiza katika biashara za namna hiyo na kwamba upelelezi kuhusu kampuni hiyo utakapokamilika wahusika watafikishwa mahakamani.

Watano Azam FC kuikosa Ruvu Shooting
Kocha Kaze aitumia salamu Dodoma Jiji FC