Baraza la mashirikisho ya soka kusini mwa bara la Afrika (COSAFA), limemteua Ahmad Ahmad kuwa mtu pekee atakaeingia kwenye harakati za uchaguzi wa rais wa shirikisho la soka barani Afrika CAF.

Ahmad, ambaye ni rais wa chama cha soka nchini Madagascar ametajwa kusimama katika nafasi ya kuwania kiti cha ukuu wa CAF, huku akitarajia upinzani kutoka kwa rais wa sasa wa shirikisho hilo Issa Hayatou katika uchaguzi ambao umepangwa kufanyika mwezi March nchini Ethiopia.

COSAFA walipitisha jina la Ahmad, katika mkutano wao mkuu uliofanyika mjini Johannesburg nchini Afrika kusini siku ya jumamosi, ambapo asilimia kubwa ya wajumbe waliafiki jina la kiongozi huyo kuwa sehemu ya uchaguzi mkuu wa CAF.

Rais wa COSAFA Dr Phillip Chiyangwa aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo, wameafiki jina la Ahmad kuwa pekee kutoka kwenye ukanda huo, na akaahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa kiongozi huo wa soka nchini Madagascar katika harakati za kuwania kiti cha urais wa CAF.

Issa Hayatou, amekua rais wa CAF tangu mwaka 1988, na ameomba kuwania kiti hicho kwa mara ya nane mfululizo.

Kwa mara ya mwisho kiongozi huyo alichaguliwa kuwa rais wa CAF, katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2013.

Claudio Ranieri atishia kufanya mabadiliko baada ya vipigo
Wafika Polisi kuomba wapewe dawa za kulevya, ‘zimeadimika!'