Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC), imefunga mipaka yake yote na Rwanda huku hali ya mvutano kati ya nchi hizo mbili ukiendelea kuongezeka kufuatia madai ya Rwanda kuunga mkono waasi wa M23 wanaopigana na jeshi la DRC.
Mbali na uamuzi huo, mpaka wa Petit Barier ulio mjini Goma, utakuwa ukifungwa kuanzia saa tisa alasiri hadi saa moja asubuhi ili kuruhusu wafanyabiashara kufanya shughuli zao.
Awali, mwanajeshi wa DRC alivuka mpaka na kuingia Rwanda ambapo aliwashambulia kwa risasi na kuwajeruhi polisi wawili wa Rwanda kabla ya mwanajeshi huyo kupigwa risasi na kuuawa.
Wakati huo huo, Kundi la wapiganaji wa M23 limeitungua ndege ya jeshi la DRC karibu na mji wa Goma, madai ambayo yamethibitishwa na Msemaji wa waasi hao Major Willy Ngoma ambaye amesema lengo lilikuwa ni kufanya shambulizi dhidi ya wanajshi wa DRC.
Hata hivyo, Rwanda inakanusha madai kuwa inawaunga mkono waasi wa M23, ambao uongozi wao unatoka katika kabila moja la Kitutsi kama la Rais wa Rwanda Paul Kagame anayehisiwa kutuma wanajeshi mashariki mwa nchi hiyo ya DRC.