Kiungo wa klabu bingwa nchini England Leicester City Daniel Noel “Danny” Drinkwater, huenda akaihama klabu hiyo kabla ya dirisha la usajili halijafungwa mwishoni mwa mwezi huu.

Drinkwater, alikua chagizo kubwa katika kikosi cha Leicester City msimu uliopita na kufanikisha azma ya kuandika historia ya kutwaa ubingwa wa nchini England kwa mara ya kwanza.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26, ameibua hali ya sintofahamu huko King Power Stadium baada ya kugoma kusaini mkataba mpya, kwa kigezo cha kutofurahishwa na ofa ya mshahara ambao anapaswa kulipwa kwa juma.

Uongozi wa The Foxes umemtayarishia mkataba Drinkwater, ambao utamuwezesha kulipwa mshahara wa Pauni 80,000 kwa juma, kiasi ambacho anaamini hakiendani na thamani yake kwa sasa.

Hata hivyo uongozi wa Leicester City, umeripotiwa kujipanga upya na kuangalia uwezekano wa kumuongezea dau la mshahara Drinkwater, hadi kufikia Pauni 100,000 kwa juma.

Kutokana na mvutano huo, gazeti la The Sun limeandika kuwa, uongozi wa       klabu ya Tottenham Hotspur, umejipanga kutumia udhaifu uliopo ili kufanikisha suala la kumnasa Drinkwater, katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

Tayari Spurs wameonyesha nia ya kutaka kuwasilisha ofa ya kumsajili kiungo huyo na taarifa za awali zinaeleza kwamba, endapo Drinkwater atakubali kuelekea kaskazini mwa jijini London atakua akilipwa mshahara wa zaidi ya Pauni 100,000 kwa juma.

Alexandre Lacazette Kumrejesha Nyumbani Loic Remy
Mvutano Wa Ada Ya Usajili Wavuruga Mipango Ya Inter Milan