Droo ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup – ASFC), inatarajiwa kufanyika kesho Jumatano Desemba 06, 2017 kwenye Studio za Kituo cha Televisheni cha Azam, kilichopo Tabata relini, Dar es Salaam.

Droo hiyo itakayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Mdhamini wa michuano hiyo – Kituo cha Televisheni cha Azam, itachezeshwa na wachezaji wanne wa zamani.

Wachezaji hao watakaoshuhudiwa na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari na viongozi wa timu husika, ni makipa wa zamani wa Taifa Stars ya Tanzania, Mohammed Mwameja na Steven Names kadhalika Mabeki George Masatu na Kanneth Mkapa.

Michuano hiyo ambayo Bingwa Mtetezi ni Simba SC ya Dar es Salaam, ilianza kwa kushirikisha timu 91, lakini kwa sasa zimebaki timu 64 tu ambazo zinaingia kwenye droo hiyo ya kesho.

Timu 91 maana yake ni kwamba zilikuwa 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL); 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL); 24 za Ligi Daraja la Pili (SDL) na 27 za Ligi ya Mabingwa wa Mkoa (RCL). Timu 27 zimeondolewa katika hatua ya awali na ya kwanza.

Wachezaji hao wa zamani watakuwa na kazi ya kuchagua vitufe kwa timu ya nyumbani na ugenini katika mechi zitakazochezwa Desemba 22, 23, 24 na 26.

Timu zinazoingia kwenye droo Buseresere ya Geita, Ambassodor ya Kahama mkoani Shinyanga na Eleven Stars ya Kagera, AFC ya Arusha,  Bodaboda FC pamoja na Area C FC na Mji Mkuu FC za Dodoma wakati timu nyingine ni mshindi kati ya New Generation na Sahale All Stars.

Nyingine ni  Green Warriors, Villa Squad FC, Ajabalo FC, Reha FC za Dar es Salaam, Milambo ya Tabora, Majimaji Rangers ya Nachingwea mkoani Lindi pamoja na Kariakoo ya Lindi.

Pia zimo Shupavu FC ya Morogoro, Ihefu FC ya Mbeya, Makanyagio ya Rukwa, Burkina FC ya Morogoro, Makambako Heroes ya Njombe, Real Moja Moja, Boma FC ya Mbeya, Pepsi ya Arusha na Madini FC pia ya Arusha.

Timu za Ligi Daraja la Kwanza zinazoingia kwenye droo ni African Lyon, Ashanti United, Friends Rangers za Dar es Salaam, JKT Ruvu na Kiluvya United za Pwani, Mgambo JKT ya Tanga, Mvuvumwa ya Kigoma na Polisi Tanzania ya Morogoro.

Nyingine ni Coastal Union ya Tanga; JKT Mlale ya Ruvuma; KMC ya Dar es Salam, Mawezi Market ya Morogoro, Mbeya Kwanza ya Mbeya, Mufundi United ya Iringa, Mshikamano na Polisi Dar za Dar es Salaam, Alliance School, Pamba na Toto African za Mwanza, Rihno Rangers ya  Tabora, Transit Camp ya Shinyanga na JKT Oljoro ya Arusha.

Timu za Ligi Kuu ni pamoja na Young Africans, Simba na Azam FC za Dar es Salaam; Ruvu Shooting ya Pwani, Mtibwa Sugar ya Morogoro, Lipuli ya Iringa, Njombe Mji ya Njombe, Majimaji ya Songea mkoani Ruvuma na Ndanda ya Mtwara.

Nyingine ni Stand United na Mwadui za Shinyanga; Tanzania Prisons na Mbeya City FC za Mbeya; Mbao FC ya Mwanza, Kagera Sugar ya Kagera na Singida United ya Singida.

Kili Stars yajifua, Ninje akubali
Meya wa Ubungo: Mnyika hang'oki Chadema