Uongozi wa DTB FC (Singida Big Stars) umekanusha taarifa za kuwa mbioni kumuajiri Mwinyi Zahera ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soka la vijana Young Africans.
Afisa Mtendaji Mkuu wa DTB FC (Singida Big Stars) Muhibu Kanu amesema, taarifa za Mwinyi Zahera kuwa kwenye mipango ya klabu hiyo sio za kweli, na wao wameshtushwa kuziona kwenye mitandao ya kijamii.
Amesema Uongozi wa klabu hiyo itakayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao una taratibu zake za kuajiri nafasi mbalimbali, na hauna utaratibu wa kusambaza taarifa zake kabla ya mambo kukamilika.
“Hata sisi tunaona na kuzisoma hizo taarifa zinazoenea kwenye mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari kwamba tumemsaini Mwinyi Zahera kuwa Kocha Mkuu kwenye timu yetu”
“Ukweli ni kwamba, bado bodi haijakaa na kukubaliana ni nani anaweza kuja kuwa Kocha Mkuu”
“Tunachokifanya sasa hivi ni kupitia ripoti ya Kocha inaeleza nini, nani asajiliwe, wale tuliokuwanao tangu Championship nani abaki nani tumruhusu aondoke”
“Kama malengo ya msimu ujao yatamhitaji Kocha Zahera basi tutamtafuta na kuzungumza nae halafu tukikubaliana tutampa mkataba”
“Endapo malengo yetu hayamhitaji Kocha mwingine sio Zahera, basi tutamtafuta mahali popote alipo aje kufanya kazi.” Amesema Muhibu Kanu