Kocha Mkuu wa Azam FC Abdihamid Moallin, amesema ameamua kumbadilishia nafasi Mshambuliaji wake kutoka Zimbabwe Prince Dube, kutokana na uhitaji wa kikosi chake kwa sasa.
Moallin aliyerithi mikoba ya Kocha kutoka nchini Zambia George Lwandamina, amesema asili ya Dube ni Mshambuliaji wa kati, lakini ameamua kumbadili na kuanza kumtumia kama Mshambuliaji anayetokea Pembeni.
Amesema naamini nafasi hiyo itamuwezesha Dube kuwa na uwezo wa kuisaidia Azam FC, tofauti na alivyokua amezoeleka, hivyo amewasihi Mashabiki wa klabu hiyo kutarajia mabadiliko yatakayoleta tija kikosini kwake.
“Baadhi ya michezo Dube alicheza kama mshambuliaji wa kati lakini kutokana na ushindani mkubwa uliopo nimeamua kumbadilisha na kumpeleka pembeni ili aweze kuisaidia timu,” amesema Kocha Moallin na kuongeza;
“Ni mshambuliaji mzuri na nina imani kubwa kwake licha ya siku za hivi karibuni kupitia kipindi kigumu cha timu kutopata matokeo, hilo ni jukumu langu kumfanya kuendeleza ubora wake na kuanzia sasa tutaona mabadiliko.”
Dube alianza msimu huu vibaya kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, lakini pamoja na kuanza kucheza kwenye kikosi cha Azam FC, mambo yameendelea kuwa magumu kwake, kwani ameshindwa kufunga.