Wachezaji Prince Dube, Never Tigere na Bruce Kangwa wataukosa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba SC dhidi ya Azam FC utakaopigwa Jumamosi (Januari Mosi 2022), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Wachezaji hao wamerejea nchini kwao Zambabwe na kujiunga na kikosi cha nchi hiyo kilichoanza kambi ya kujiandaa na Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2022’.

Tayari wachezaji hao wameshaanza mazoezi na wachezaji wenzao mapema leo Jumatatu (Desemba 27) mjini Harare, na kukosekena kwao kwenye mchezo dhidi ya Simba SC, huenda kukalifanya Benchi la Ufundi la Azam FC kuwaibua wachezaji wengine ambao huenda wakafanya vizuri.

Simba SC itakua mwenyeji katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa soka nchini, hasa baada ya timu hizo kupata ushindi wa mabao manne kwenye michezo iliyopita.

Simba SC iliifunga KMC FC mabao 4-1 ugenini mjini Tabora katika Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi, huku Azam FC wakiifunga Ruvu Shooting mabao 4-1 jijini Dar es salaam kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 21, huku Azam FC, ambayo imeshashuka dimbani mara 10 msimu imejikusanyia alama 15 zinazoiweka nafasi ya saba.

Baada ya mchezo huo, Simba SC, Young Africans, Azam FC na Namungo FC zitaelekea Zanzibar tayari kwa michuano ya Mapinduzi Cup inayotarajiwa kuanza Jumapili (Desemba 02).

Simba SC ipo Kundi C pamoja na Selem View na Mlandege FC, wakati Kundi B, linaundwa na Young Africans, Taifa Jang’ombe na KMKM SC huku Kundi A likiwa na Azam FC, Namungo, Yosso Boys na Meli 4 City.

Rais Mnagangwa ampongeza dereva wa lori
Mbeya Kwanza FC yawaita Young Africans mezani