Wakati Joto la pambano la ngumi kati ya Bondia Abdallah Pazi ‘Dula Mbabe’ na Erick Katompa kutoka DR Congo likizidi kupanda, Promota wa pambano hilo, Sophia Mwakagenda, amesema lengo la pambano hilo ni kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii wa ndani.
Mwakagenda amesema lengo la pambano hilo ni kutangaza utalii kama alivyofanya Rais Samia kupitia filamu ya Royal Tour, na pambano hilo litashuhudiwa na watu kutoka ndani na nje ya nchi.
Mwakagenda ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum, amesema wamepeleka pambano hilo katika Jiji la Arusha kwa sababu kipindi hicho ni msimnu wa utulivu kwa watalii wanaotembelea Tanzania, hivyo miongoni mwa vitu watakavyopata ni burudani ya ngumi.
Amesema pambano hilo litafanyika Novemba 25 mwaka huu na linatajwa kuwa la kihistoria na kulipa kisasi.
“Pambano hilo litatanguliwa na mapambano mengine ya utangulizi tisa na watakaopanda ni wapiganaji wakali wakiwemo wanawake, kwa hiyo hakuna atakayejuta kufika kwenye uwanja wa vitasa, naomba watu wajitokeze, amesema Mwakagenda.
Kuhusu mshindi kupewa jina la mnyama, amesema mbali na zawadi nono ambayo mshindi ataibuka nayo, lakini atakuwa na nafasi ya kuchagua jina la mnyama anayemtaka na litalipiwa kwa niaba yake kama alama ya utambulisho kwa nchi.
Mwakagenda amesema kuwa mabondia kabla na baada ya mapambano yao watapata nafasi ya kutembelea mbuga za wanyama kuangalia vivutio ili wawe sehemu ya kuutangaza utalii wa nchi.