Uongozi wa FC Barcelona umefikia makubano na mshambuliaji kinda Anssumane “Ansu” Fati Vieira, ambayo yatazinufaisha pande hizo mbili kwa maslahi ya klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania *La Liga*.
Pande hizo mbili zimekubaliana kuboresha mkataba hadi Juni 30, 2024, na yoyote atakaehitaji kuuvunja atapaswa kulipa kiasi cha Euro Milioni 170 ambacho kitakua kikipanda hadi Euro Milioni 400.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 17 amekuwa mmoja wa nyota waliowika sana Barani Ulaya msimu uliopita na anatajwa kuwa na mustakabali mzuri kwenye kikosi cha FC Barcelona.
Kifungu cha awali kwenye Mkataba wa Kinda huyo kilikuwa Euro Milioni 100 kikapanda hadi Euro Milioni 170, na yaliwekwa makubaliano kwamba wakati mchezaji huyo atakapoingia rasmi katika kikosi cha kwanza cha Barça kifungu kitaboreshwa hadi Euro Milioni 400.
Ansu Fati ambaye ni mzaliwa na Guinea-Bissau alianza kutumika kwenye kikosi cha wakubwa cha FC Barcelona mwaka 2019, baada ya kukuzwa na kuendelezwa kisoka kwenye kituo cha vijana cha klabu hiyo (La Masia).
Ameshacheza michezo 24 na kufunga mabao saba, na jambo lingine alilolifanya kwenye historia ya maisha yake kisoka ni kukubali kuitumikia Hispania na kulikacha taifa la Guinea-Bissau.
Upande wa timu ya taifa ya vijana ya Hispania chini ya umri wa miaka 21, Ansu Fati ameshacheza michezo miwili, huku akicheza michezo miwili kwenye timu ya taifa ya wakubwa na kufunga bao moja kati ya mwaka 2019-20.