Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimehimizwa kuendelea kuunga mkono jitihada za kujikwamua kiuchumi zinazofanywa na Wajasiriamali wadogo na wa kati, ili kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana na wanawake na kukuza uchumi wa nchi hizo.

Rai hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Burundi, Prosper Bazombaza jijini Bujumbura, Burundi wakati akifungua rasmi Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayoendelea jijini hapa kuanzia Desemba 5-15 2023.

Amesema Nchi Wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaweza kujikwamua katika changamoto ya ajira kwa vijana na wanawake kwa kuandaa mazingira yanawezesha makundi hayo kujiajiri ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha na kuboresha Maonesho ya Wajasiriamali wadogo ili kuwa na tija zaidi kwa maslahi ya Wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maoenesho hayo, Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania ambaye pia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha Wajasiriamali 259 wa Tanzania kushiriki Maonesho hayo.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Gelasius Byakanwa amewapongeza na kuwashukuru Wajasiriamali walioshiriki maonesho hayo na kutoka wito kwa wajasiriamali wengine kuendelea kushiriki maonesho hayo kwani ni fursa ya kuyafikia masoko na kupata uzoefu na kujifunza ubunifu kutoka kwa wajasiriamali wengine wanaoshiriki.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na Biashara, Annette Mutaawe ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo kwenye ufunguzi wa maonesho hayo amesema kuwa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo
itaendelea kuboresha maonesho hayo ambapo wajasiriamali hao wanachangia kupunguza changamoto ya ajira kwa asilimia 65 na pato la kanda kwa asilimia 15.

Akizungumza kwa niaba ya Wajasiriamali hao, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati Afrika Mashariki, Josephat Rweyemamu amezishukuru Serikali zinazounda Nchi Wanachama kwa kuwewawezesha kushiriki na kusisitiza umuhimu wa nchi wanachama kufanyia kazi changamoto chache zilizopo ili kuboresha biashara miongoni mwa watu wake ikiwemo kuwa na sarafu
moja ili kurahisisha biashara pamoja na kuendelea kukuza lugha ya Kiswahili kwa kukifanya kuwa lugha ya biashara.

Uhuru wa Tanganyika: Kilimanjaro hawakujua maana
Picha: Rais Samia katika maadhimisho Miaka 62 ya Uhuru