Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki amesema wanaendelea na mchakato wa kuhakikisha amani inapatikana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC), kwakuwa nchi hiyo ni mwanachama kamili wa jumuiya hiyo hivyo anastahili kusaidiwa kwenye masuala ya usalama.
Akihojiwa jijini New York, Marekani wakati wa mjadala mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77 Dkt Mathuki amesema pamoja na kupokea ombi kutoka Serikali ya DRC ya kupeleka majeshi Mashariki mwa nchi hiyo lakini hilo litafanyika pale tu iwapo mazungumzo yatashindikana.
Amesema “Wakati nilipotembelea kinshasa ilikuwa miongoni mwa majukumu yangu ni pamoja na kusaini mkataba wa SOFA baina ya DRC na jumiya ya Afrika Mashariki, mkataba huu unaruhusu majeshi ya nchi wanachama kwenda DRC kwa ajili ya kuwasaidia kuhakikisha wana amani na kuondoa shida ambazo zipo nchini humo.”
Mkataba huu wa SOFA, unaeleza majukumu ya jeshi la kikanda katika eneo la DRC na uwezeshaji na usaidizi utakaotolewa na Serikali ya nchi mwanachama kwa mujibu wa Katiba na sheria zinazotumika katika jumuiya ya Afrika Mashariki huku akisema, pamoja na kusaini mkataba huo pia walikubaliana kuwa na njia mbili za kumaliza mzozo wa Mashariki mwa DRC
Dkt. Mathuki amesema, “La kwanza na muhimu zaidi ni la kidiplomasia na kisiasa, na hii inamaanisha tunakaa chini na kufanya mazungumzo kwa pamoja kuona hali ipoje, nini kifanyike, na kuelewesha shida gani hasa ipo na jinsi ya kuiondoa changamoyto zinazowakabili wananchi walioko DRC.”
Aidha, Mathuki pia alifanya kikao na Rais wa DRC, Felix Tshisekedi ambaye alikuwa miongoni mwa marais waliozungumza siku ya kwanza ya ufunguzi wa mjadala wa wazi wa Baraza Kuu na kuwasilisha ombi lake kwa Nchi za Afrika Mashariki kupeleka wanajeshi Mashariki mwa nchi hiyo eneo ambalo kwa zaidi ya miaka 20 limekuwa na mzozo.