Katika kuhakikisha ugonjwa wa Ebola hauingii nchini serikali kupitia wizara ya Afya kwa kushirikiana na watalaam mbalimbali wa afya ngazi ya mitaa hadi taifa wameendelea kutoa elimu hiyo mkoani Kagera.
Baada ya hivi karibuni kuripotiwa visa vya ugonjwa huo nchini Uganda, mganga mkuu mkoa wa Kagera Dkt. Issessanda Kaniki ametembelea mitaa mbalimbali mjini Bukoba ikiwemo kituo cha mabasi Bukoba pamoja na nyumba za kulala wageni.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 10,2022 mara baada ya kufika kituo cha mabasi Bukoba, Mganga mkuu wa Mkoa wa Kagera Dkt.Issessanda Kaniki amesema hiyo ni katika mwendelezo wa kujipanga katika kukabiliana na Ebola kwa kuzingatia kanuni na masharti ya afya.
“Tumeendelea kuelimisha wananchi hasa abiria katika tishio hili la ugonjwa wa Ebola pia tumeendelea kukagua miundombinu na usafi uhakika wa magari ambayo yanabeba hivyo tunahamasiha wananchi kuendelea kujikinga ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka ikiwezekana kutumia sanitizer,” amesema.
Hata hivyo, Dkt. Kaniki amesema mwitikio wa wananchi ni mkubwa katika jamii.
“Mwitikia ni mkubwa kwani kupitia kwa viongozi wa serikali za mitaa na watoa huduma ngazi ya jamii nao wamekuwa wakipita nyumba hadi nyumba kuhakikisha elimu elimu ya Ebola inafika kwa kila mtu,”amesema.
Nao baadhi ya wananchi wakiwemo makondakta na madereva katika kituo cha mabasi Bukoba wamesema hatua ya serikali kuweka kipaumbele utoaji wa elimu ya Ebola kabla ya madhara kutokea ina umuhimu mkubwa katika kunusuru afya kwa jamii.
“Pamoja na kwamba Tanzania hatujapata Ebola nawasihi watanzania tuendelee kutii maelekezo ya serikali kwani ina nia njema ya kutulinda tufuate kanuni za afya,” amesema Shakilu Adam.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Moses Machali amesema wao kama wilaya wamejipanga kuwa na vifaa tiba vya kutosha ambapo pia kuna eneo maalum limetengwa kwa ajili ya matibabu iwapo kuna mtu atabainika kuwa na maambukizi ya Ebola.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amesema wilaya imejipanga kuzuia Ebola katika matukio mbalimbali yanayokutanisha watu ikiwemo tukio la uzimaji wa mwenge kitaifa Oktoba 14,2022.
Ikumbukwe kuwa tangu visa vya Ebola viripotiwe nchini Uganda, Tanzania bado ipo salama ila imekuwa mstari wa mbele kwa kuchukua tahadhari mapema katika kuhakikisha wananchi wake wanakuwa salama na wanaendelea na majukumu yao ya kila siku.