Kocha Mkuu wa Newcastle, Eddie Howe ametamba kuwa na kikosi bora msimu huu baada ya kuindosha Manchester City inayonolewa na Kocha Pep Guardiola, katika michuano ya Kombe la Carabao.

Newcastle iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Manchester City, katika mchezo uliofanyika juzi Jumatano (Septemba 27) Uwanja wa St James’ Park, timu hiyo ikitinga raundi ya nne ya michuano hiyo.

Katika mchezo huo, bao pekee liliwekwa kimiani na mshambuliaji Alexander Isak katika dakika ya 53 kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Joelinton.

Newcastle, iliyopoteza mechi ya fainali msimu ulipita mbele ya Manchester United, Kocha Howe alifanya mabadiliko kwa wachezaji 10 waliotumika katika mchezo wa Ligi Kuu ya England mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Sheffield United, timu yake ilipoibuka na ushindi wa mabao 8-0.

Kocha Howe, alisema katika msimu huu wana kikosi bora zaidi ya msimu uliopita baada ya kufanya usajili wa wachezaji wanaounda timu ya ushindani.

“Nimefurahishwa na kitendo cha kupata ushindi mbele ya Manchester City kwani msimu huu tuna kikosi bora cha ushindani na lengo ni kufika mbali ikiwemo kubeba Kombe la Carabao.

Tunatambua bado tuna kazi kubwa ya kufanya katika michuano hiyo msimu huu, lakini tutapambana kwa kila namna kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Kocha Howe.

Alisema hata hivyo wachezaji wake walionyesha kiwango bora kwa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu katika mchezo huo.

Utunzaji wa Mazingira: REA, Oryx wagawa mitungi 3600
Msimu wa sita maonesho Women Gala wazindiliwa