Gazeti la The Sun la nchini England limeibua tetesi kuhusu mustakabali wa kiti cha umeneja cha klabu ya Arsenal ambacho kwa sasa kinakaliwa na meneja Arsene Wenger ambaye yu njiani kuondoka.

Gazeti hilo maarufu nchini humo ambalo linamili tovuti ya SunSport limeibua tetesi hizo kwa kumtaja meneja wa klabu ya Bournemouth Eddie Howe kama mbadala wa mzee huyo kutoka nchini Ufaransa.

Taarifa zilizochapishwa kwenye tovuti ya gazeti hilo zimeeleza kuwa, jina la Eddie Howe limekua likitajwa mara kwa mara na viongozi wa Arsenal katika baadhi ya vikao vyao, kwa kuona huenda akawa mtu sahihi kuwa meneja mpya klabuni hapo.

Eddie Howe ameonyesha kuwa na mtazamo tofauti katika ufundishaji wake tangu alipofanikiwa kuipandika daraja Bournemouth, akiitoa ligi daraja la kwanza msimu wa 2014/15 na kucheza ligi kuu msimu uliofuata.

Jambo hilo linatajwa kuwa kishawishi kikubwa kwa viongozi wa Arsenal ambao wanaamini aina ya soka analolifundisha meneja huyo kutoka nchini England litakidhi haja ya The Gunners ambao hupendelea utamaduni wa kumiliki mpira kwa muda mrefu wanapokua uwanjani.

Arsene Wenger anatarajiwa kuondoka Emirates mwishoni mwa msimu huu kufuatia mkataba wake kuelekea ukingoni, hivyo uongozi wa klabu hiyo ya kaskazini mwa jijini London umeanza mchakato wa kuangalia nani atafaa kuwa mbadala wake.

Hata hivyo kuna tetesi zinazodai kuwa, tayari Wenger ameanza kubadili mawazo ya mpango huo, na ameshamueleza muwekezaji mkuu wa Arsenal Stan Kroenke kuwa, angependa kusaini mkataba mpya.

Ilkay Gundogan Afikiriwa Kucheza Dhidi Ya Man Utd
Safari Ya Urusi 2018: Brazil Yachanja Mbuga