Shirikisho la soka Saudi Arabia (SAFF) limemtangaza muagentina Edgardo Bauza kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo ambayo imefuzu kucheza fainali za kombe la dunia zitakazofanyika Urusi.
Maamuzi ya SAFF kumtangaza kocha huyo, yamekuja kutokana na kumalizika kwa mkataba wa kocha mdachi Bert van Marwijk.
Van Marwijk, amekua kocha wa kikosi cha Saudi Arabia tangu mwaka 2015, na alifanikisha jukumu la kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri katika harakati za kuwania fainali za kombe la dunia za 2018.
Kwa sasa Saudi Arabia imefanikiwa kufuzu fainali hizo, ikitokea kundi B sambamba na Japan huku wakiiacha Australia ikienda katika mzunguuko wanne wa kufuzu.
Bauza ambaye alikua kocha mkuu wa timu ya taifa ya Argentina kuanzia 2016-17, atakua na kazi ya kuiwezesha nchi hiyo ya barani Asia kupambana vilivyo kwenye fainali za kombe la dunia na kufikia lengo la kufanya vizuri.
Kwa mara ya mwisho Saudi Arabia walishiriki fainali za kombe la dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani.