Mshambuliaji wa Paris Saint-Germain, Edinson Cavani (Pichani) ameula baada ya kutangaza kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa ligi daraja la kwanza nchini Ufaransa maarufu kama Ligue 1, katika hafla iliyofanyika usiku wa kuamkia leo.
Cavani mwenye umri wa miaka 30, ametwaa tuzo hiyo baada ya kuifungia Paris Saint-Germain mabao 48 kwenye michuano yote msimu huu.
Mabao 35 yakiwa ni ya Ligue 1 na kuwa karibu kuvunja rekodi ya mabao 50 iliyowekwa msimu uliopita na Zlatan Ibrahimovic.
Nafasi ya pili imechukuliwa na Bernardo Silva wa AS Monaco huku nafasi ya tatu ikienda kwa Alexandre Lacazette wa Lyon. Katika hatua nyingine, tuzo ya mchezaji bora wa kike imekwenda kwa Sakina Karchaoui wa Montpellier.
Nyota wa AS Monaco, Kylian Mbappe ametangazwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora chipukizi baada ya msimu huu kufunga mabao 14 na kupika mengine 11.
Ikumbukwe Mbappe mwenye umri wa miaka18, amekuwa muhimili mkubwa kwa AS Monaco, akiisaidia timu hiyo kufika nusu fainali ya michuano ya klabu bingwa Ulaya na kuongoza Ligue 1.
Tuzo ya kocha bora wa msimu imekwenda kwa Leonardo Jardim wa AS Monaco, huku tuzo ya kipa bora ikienda kwa Danijel Subasic pia wa AS Monaco.
Kiungo wa Chelsea, N’Golo Kante amechaguliwa mchezaji bora wa msimu wa Ufaransa kwa wachezaji wanaocheza nje. Msimu uliopita tuzo hiyo ilikwenda kwa Antoine Griezmann.
Tuzo ya bao bora la msimu imeenda kwa winga wa zamani wa Manchester United, Memphis Depay ambaye kwa sasa anaichezea Lyon.
Kikosi bora cha Msimu (4-3-3): Danijel Subasic (Monaco), Djibril Sidibe (Monaco), Kamil Glik (Monaco), Thiago Silva (PSG), Benjamin Mendy (Monaco), Jean-Michael Seri (Nice), Marco Verratti (PSG), Bernardo Silva(Monaco), Alexandre Lacazette (Lyon), Edinson Cavani (PSG) na Kylian Mbappe (Monaco).