Mshambuliaji wa klabu bingwa nchini Ufaransa Paris Saint-Germain Edinson Cavani ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya mguu wa dhahabu, katika hafla iliyofanyika mjini Monaco.
Cavani ameshinda tuzo hiyo baada ya kukidhi vigezo vyote ambavyo, vinamuwezesha kuwapiku magwiji Cristiano Ronaldo, Luis Suarez na Lionel Messi, ambao walidhaniwa huenda mmoja wao angeibuka kidedea.
Tuzo hiyo ambayo huratibiwa na World Champions Club, hutolewa kwa mchezaji mwenye nidhamu, ushirikiano na msaada mkubwa kwa timu/klabu anayoitimikia, na anapaswa kuwa na umri wa miaka 28 ama zaidi.
Cavani mwenye umri wa miaka 31, alionyesha uwezo mkubwa kisoka msimu uliopota, kwa kuisaidia PSG kutwaa ubingwa wa Ufaransa pamoja na kufika hatua ya 16 bora ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, kabla ya kutolewa na Real Madrid.
Cavani alianza safari yake ya soka la ushindani akiwa nchini kwao Uruguay katika klabu ya Danubio, kabla ya kutimkia barani Ulaya kujiunga na Palermo ya Italia mwaka 2007.
Tuzo ya mguu wa dhahabu (Golden Foot Award).
Tangu msimu wa 2008-09, amekua akionyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao zaidi ya kumi, akiwa na klabu za Palermo, Napoli, pamoja na mabingwa wa soka nchini Ufaransa (French Ligue 1) PSG, ambapo tayari ameshafanikiwa kutwaa mataji manne.
Cavani pia ameshaifungia timu yake ya taifa mabao 46 katika michezo 106 aliyocheza, na amefanikiwa kutwaa ubingwa wa mataifa ya kusini mwa Amerika (Copa America) mwaka 2011.
Waliokua wakiwania tuzo ya mguu wa dhahabu mwaka huu 2018.
Manuel Neuer (Germany, Bayern Munich), Lionel Messi (Argentina, Barcelona), Cristiano Ronaldo (Portugal, Juventus), Luis Suarez (Uruguay, Barcelona), Edinson Cavani (Uruguay, PSG), Gareth Bale (Wales, Real Madrid), Sergio Ramos (Spain, Real Madrid), Robert Lewandowski (Poland, Bayern Munich), Sergio Aguero (Argentina, Man City) na Thiago Silva (Brazil, PSG).
Waliowahi kushinda tuzo ya mguu wa dhahabu tangu mwaka 2003.
2003 Roberto Baggio (Italy, Brescia), 2004 Pavel Nedvěd (Czech Republic, Juventus), 2005 Andriy Shevchenko (Ukraine, Milan) , 2006 Ronaldo (Brazil, Real Madrid), 2007 Alessandro Del Piero (Italy, Juventus), 2008 Roberto Carlos (Brazil, Fenerbahçe), 2009 Ronaldinho (Brazil, Milan), 2010 Francesco Totti (Italy, Roma), 2011 Ryan Giggs (Wales, Manchester United), 2012 Zlatan Ibrahimović (Sweden, PSG), 2013 Didier Drogba (Ivory Coast, Galatasaray), 2014 Andrés Iniesta (Spain, Barcelona), 2015 Samuel Eto’o (Cameroon, Antalyaspor), 2016 Gianluigi Buffon (Italy, Juventus) na 2017 Iker Casillas (Spain, Porto)