Mchambuzi wa Michezo nchini Tanzania Edo Kumwembe amesema Simba SC ina nafasi kubwa ya kushinda mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika Hatua ya Makundi dhidi ya ASEC Mimosas.
Simba SC itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa ‘Kundi D’ siku ya Jumapili (Februari 13), utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kuanzia majira ya saa kumi jioni.
Kumwebwe ambaye pia ni Mwandishi wa Habari za Michezo Mwandamizi ametoa uhakika huo alipokua kwenye kipindi cha Sports Arena cha Wasafi FM leo Alhamis (Februari 10).
Kumwembe amesema Simba SC inachotakiwa kukifanya siku ya mchezo ni kupambana kwa malengo kama ilivyokua inafanya kwenye michezo ya kimataifa waliyoshinda Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam.
Amesema uwezo wa klabu za Afrika Magharibi kwa sasa ni wa kawaida, tofauti na ilivyokua miaka 20 iliyopita, ambapo ukanda huo ulikua umetawala soka la Barani Afrika.
“Simba SC wasitishwe na ASEC Mimosas, kwa sababu klabu za West Africa sio imara kama ilivyokua zamani, ni miaka mingi imepita kwa klabu za ukanda huo kucheza soka la ushindani, hivyo Simba SC wanachotakia kukifanya ni kujiamini na kucheza soka lao kama walivyofanya katika michezo waliyoshinda Kwa Mkapa.”
“Klabu ya West Africa zilisumbua sana miaka 20 iliopita, sio kwa sasa, ambapo hata kwenye orodha ya klabu bora Barani Afrika zinatokea kwa kubahatisha sana, binafsi naamini Simba SC itashinda Jumapili.” amesema Kumwembe.
Simba SC imepangwa Kundi D na klabu za ASEC Mimosas (Ivory Coast), RS Berkane (Morocco) na US Gendermarie (Niger).