Mwandishi wa Habari za Michezo Mwandamizi Edo Kumwembe amewashangaa baadhi ya Viongozi wa zamani wa Simba SC ambao wanapambana kuwaaminisha Mashabiki na Wanachama kuwa timu yao ni mbovu.
Simba SC imepoteza mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, na itamaliza msimu huu ikiwa na taji la Mapinduzi pekee.
Kumwembe ambaye pia ni Mchambuzi wa Michezo wa Kituo cha Wasafi Media amesema anaashangazwa kuona baadhi ya viongozi wa zamani wa klabu hiyo wakitumia nafasi ya kushindwa kutwaa mataji kwa kigezo kisichokua na mantiki.
Amesema Simba SC haijafanya vibaya kama inavyoelezwa na Viongozi hao wa zamani, zaidi ya kutafuta sababu za kuwaaminisha watu kwa kuifananisha klabu hiyo kama Tanzania Prisons ambayo haina matokeo mazuri msimu huu.
“Vile naangalia baadhi ya Viongozi wa zamani wa Simba wakipambana kuivunja timu yao wanahaha kweli kweli nilidhani katiba mpya walio ipitisha itaondoa haya mambo, Aah wapi.
“Simba wanamaliza wa pili katika ligi, robo fainali katika Shirikisho barani Afrika na nusu fainali katika FA. Lakini watu wanataka ionekane imefanya vibaya kama Prisons tu.” amesema Kumwembe
Mwenyekiti wa Kamati ya usajili Kassim Dewji na Mjumbe wa Bodi Mwina Kaduguda ni sehemu ya viongozi ambao wameonesha kuwa tofauti na kinachoendelea Simba SC.