Young Africans imeendelea kutabiriwa Ubingwa wa Tanzania Bara Msimu huu 2021/22, huku ikiendelea kuongoza msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya alama tano.
Young Africans ambayo inahaha kuusaka ubingwa wa Tanzania Bara kwa misimu minne mfululizo, huku Watani Zao wa Jadi Simba SC wakiwa kwenye furaha ya Ubingwa wamekua na kikosi kizuri msimu huu ambacho kinawaaminisha wadau wengi wa soka kuwa, wana nafasi ya kumaliza ukame unaowakabili.
Mchambuzi wa Michezo nchini Tanzania Edo Kumwembe amekuwa mmoja wa wadau ambao wanaamini msimu huu Young Africans itatawazwa kuwa Bingwa kutokana na faida kubwa ya kucheza michezo mingi ugenini katika Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi Kuu ambao unafungwa rasmi leo Jumatano (Februari 23).
Young Africans itakua mgeni wa Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa Mzunguuko wa 15 ambao utapigwa Mkoani Morogoro, Wilayani Mvomero yalipo makao makuu ya wenyeji wao Mtibwa Sugar, katika Uwanja wa Manungu Complex.
Edo Kumwembe ambaye pia ni Mwandishi wa Habari za Michezo amesema: “Young Africans itatwaa ubingwa msimu huu kwa kunufaika kucheza michezo mingi ugenini katika Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi Kuu, Michezo watakayocheza Uwanja wa Mkapa Mzunguuko wa Pili itakua rahisi sana kwao.”
Kabla ya mchezo wake dhidi ya Mtibwa Sugar leo Jumatano (Februari 23), Young Africans inaendelea kuwa na alama 36 kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, ikifuatiwa na Mabingwa Watetezi Simba SC wenye alama 31.