Klabu ya Atletico Madrid inapanga kumwongeza mkataba kocha Diego Simeone hadi mwaka 2027, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Relevo.
Kocha huyo wa kimataifa wa Argentina amebakiza mwaka huu tu, ambao utamalizika mwisho wa msimu na baada ya kuanza vizuri msimu huu, klabu imeamua kumpa mkataba mpya ambao utamfanya awepo kwa muda wa miaka 12.
Simeone alianza kuwa kocha wa Atletico Desemba 2011 na ameipatia mafanikio klabu hiyo, hivyo mabosi hawataki kumuachia kirahisi kwani amekuwa na mchango mkubwa.
Aidha, uwezekano wa Simeone kuongeza mkataba mpya bado haujathibitishwa rasmi, lakini anatarajia kukatwa mshahara endapo atasaini.
Hiyo ni kutokana na kukosa mkwanja wa Ligi Mabingwa Ulaya kutokana na Atletico kutolewa mapema katika michuano hiyo msimu uliopita 2022/23.
Simeone ameiongoza Atletico kuvuna pointi l6 msimu huu huku Atletico ikipoteza mechi moja ya La Liga.
Simeone alipongezwa kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya mahasimu wao Real Madrid mwezi uliopita huku ikionyesha kiwango bora.
Huo unakuwa ushindi mkubwa kwa Atletico chini ya Simeone msimu huu baada ya kucheza mechi saba na imejikita katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania ikiwa na Pointi 16 ikizidiwa Pointi tano dhidi ya Real Madrid ambayo ipo kileleni kwa Pointi 21.