Shirikisho la soka nchini Hispania (RFEF) limetangaza kuahirisha mchezo wa magwiji wa soka wa La Liga FC Barcelona dhidi ya Real Madrid “El Clasico” ambao ulitarajiwa kuchezwa mwishoni mwa juma lijalo (Oktoba 26) mjini Barcelona.

Taarifa ya shirikisho la soka Hispania imeeleza kuwa, sababu kubwa ya kuahirishwa kwa mchezo huo na kupelekwa mwezi Disemba, ni kufuatia zogo la kisiasa linaloendelea katika jimbo la Catalunya.

Zogo linaloendelea jimboni humo ambapo kuna mji wa Barcelona, limetokana na hukumu ya kifungo kwa viongozi tisa wa kisiasa hali iliyosabababisha kwenye jiji hilo maandamano mfululizo, jambo lililofanya mchezo huo kusogezwa mbele.

Uwanja wa Ndege wa Barcelona, El Prat ulifungwa kwa muda siku ya Jumanne kutokana na vurugu zilizoripotiwa, kufuatia watu 100 kuwekwa kizuizini tangu Jumatatu.

Karibu maofisa 200 wa polisi walijeruhiwa kwenye vurugu hizo na hivyo jambo hilo limewafanya Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) kuamua kupeleka mbele mchezo huo wa kibabe.

Kwa mantiki hiyo mpambano wa El Clasico umepangwa kuchezwa Desemba 7, na mwishoni mwa juma lijalo vigogo hao wa soka Hispania watacheza michezo ya kombe la mfalme (Copa del Rey).

Hatua ya kuahirishwa kwa mchezo wa El Clasio huenda ikawa faraja kwa meneja wa Real Madrid Zinedine Zidane, ambaye alikua kwenye muhemko wa kufutwa kazi endapo angefungwa na FC Barcelona.

Ole Gunnar Solskjaer hang'oki Manchester United
Samatta atuma salamu za ushindi Taifa Stars