Gwiji wa soka barani Afrika Essam Kamal Tawfiq El-Hadary, ametangaa kustaafu rasmi kuitumikia timu ya taifa ya Misri, baada ya kukamilisha dhumuni la kuweka historia duniani, ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa aliyeshiriki/kucheza fainali za kombe la dunia.
El-Hadary mwenye umri wa miaka 45 ametangaza maamuzi hayo, baada ya kuwa langoni mwa kikosi cha Misri kwa zaidi ya miaka 20, huku akicheza michezo 159.
Mlinda mlango huyo ambaye bado anaendelea kucheza soka akiwa na klabu ya Ismaily ya nchini kwao Misri, ataendelea kukumbukwa kufuatia mchango wake alioutoa kwenye kikosi cha Mafarao na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 1998, 2006, 2008 ana 2010.
Mwaka 2017 utaendelea kuwa katika kumbukumbu ya gwiji huyo, kufuatia kutangazwa kuwa mlinda mlango bora wa fainali za Afrika zilizofanyika nchini Gabon, licha ya kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya Cameroon kwa kufungwa mabao mawili kwa moja.
El-Hadary aliitwa katika kikosi cha Misri kilichokwenda nchini Urusi kushiriki fainali za kombe la dunia, na alifanikiwa kucheza mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Saudi Arabia, na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa aliecheza michuano hiyo yenye uzito duniani.
Katika mchezo huo, mlinda mlango huyo wa zamani wa klabu ya Al-Ahly alifanikiwa kupangua mkwaju wa penati, licha ya kikosi cha MIsri kukubali kuchwapa mabao mawili kwa moja.
Akitangaza maamuzi ya kustaafu kuitumikia timu ya taifa, mkongwe huyo alisema: “Hakuna mwanzo usio na mwisho, leo nimefikia maamuzi ya kustaafu soka la kimataifa, ninamshukuru kila mmoja aliyefanikisha ndoto zangu za kuichezea timu hii,”
“Nimefarijika kuwa sehemu ya vikosi tofauti tangu mwaka 1996, nilipoanza kuitumikia Misri, ninaamini wanaofuata baada yangu watakua wamejifunza kutoka kwangu, na mimi nitajitahidi kuwashauri pale watakapohitaji msaada wangu.”
“Tatizo ni umri, lakini kama isingelikua umri ningelitamani kuendelea kucheza katika timu ya taifa hadi mwisho wa maisha yangu hapa duniani, sina budi kukubaliana na hali halisi, kwani walikuwepo wachezaji wengine ambao walicheza kwa muda mrefu katika timu hii, lakini ulipofika muda walitangaza kustaafu.”