Mwanasoka mstaafu raia wa Senegal mwenye heshima kubwa nchini kwake, El Hadji Diouf ambaye bara la Ulaya limemjengea sifa ya kuwa mchezaji aliyekuwa ‘mtoto mkaidi’, amezungumzia hali zote mbili.
Diouf ambaye vyombo vya habari vya ulaya vilimmulika kama mchezaji aliyekuwa mkorofi tangu alipoiwakilisha nchi yake kwenye kombe la dunia mwaka 2002 nchini Japan na Korea Kusini na pia alipokuwa na Liverpool, Blackburn Rovers hadi Bolton Wanderers, amesema hatua ya kuchukuliwa kama mtu mbaya haikuwa inamtendea haki kwani yeye ni mtu mwema.
“Ilikuwa rahisi kunilenga mimi. Rahisi kumzungumzia El Hadji Diouf, waache wasema lakini mimi najua ndani ya moyo wangu ni mtu mwema. Familia yangu inajua, watu wangu wanajua, bara langu linajua mimi ni mtu mwema na hicho ndicho kitu bora zaidi. Mengine yaliyobaki sio tatizo langu,” Diouf aliiambia BBC.
Mbali na uwezo wake mkubwa kwenye soka, Diouf anakumbukwa kwa jinsi alivyokuwa mkali uwanjani na hata kuwatemea mate mara kadhaa wachezaji wa timu kadhaa na kuwazonga waamuzi.
Hata hivyo, hali ni tofauti anapokuwa nchini kwake, kila anapoonekana hadharani huzungukwa na umati wa mashabiki wake wanaompa heshima kubwa. Diouf huchukuliwa kama sehemu ya kielelezo cha mafanikio ya soka nchini Senegal.
Mchezaji huyo wa zamani ambaye amerejea rasmi kupumzika nyumbani kwao Senegal, katika jiji la Dakar amesema kuwa alikuwa akieleweka vibaya kila wakati na mfumo wa soka la Uingereza.